Benki za Kiislamu
Benki za Kiislamu ambazo hutoa huduma kama benki nyingine zinaendeshwa katika msingi wa biashara na sio ule wa riba. Benki za Kiislamu badala ya kukopesha kwa riba, hutumia rasilimali zake kwa zenyewe kujihusisha katika uzalishaji kwa kufuata misingi inayokubalika katika Uislamu. Miongoni mwa misingi inayokubalika kwa Muislamu au Benki ya Kiislamu kuingiza fedha zake katika miradi ya biashara au uzalishaji ni hii ifuatayo:


(i)Mudharabah
Mudharabah ni makubaliano kati ya watu wawili au zaidi ambapo mmoja au zaidi kati ya hao anatoa mtaji na mwingine hushiriki kwa ukamilifu katika kuendesha na kuongoza mradi wa uchumi. Faida itakayopatikana katika mradi huo itagawanywa kulingana na makubaliano yao. Hasara itakayotokana na mradi huo itakuwa ni ya mwenye kutoa mtaji. Wengine hawatoi chochote kusaidia hasara kwa sababu wameshatoa mchango wao wa hasara hiyo kwa jasho walilolitoa katika shughuli ambayo haikuzaa matunda bali hasara.Benki za Kiislamu zinaingiza fedha zake katika miradi ya uchumi kwa njia hii ya Mudharabah ambapo benki hutoa mtaji kwa ajili ya miradi mbali mbali ya uchumi kwa mapatano ya kupata kiasi (asilimia) fulani cha faida itakayopatikana na kuwa tayari kulipa hasara itakayopatikan a.


(ii)Musharikah
Musharikah ni ushiriki kati ya watu wawili ambapo, tofauti na Mudharabah wote wawili wanachangia mtaji na kushiriki katika uendeshaji wa shughuli ya kiuchumi, lakini si lazima watoe hisa sawa sawa, kwa makubaliano ya kugawana faida na hasara kulingana na kiasi cha hisa alichotoa kila mmoja wao. Kwa mtindo huu wa “Musharikah” Benki ya Kiislamu inaingia katika kuchangia mtaji, kuendesha na kusimamia mradi wa uchumi na watagawana (faida au hasara) kulingana na kiasi cha mtaji kila mmoja alichotoa.(iii)Ijara-Uara wa Iktina
Huu ni utaratibu mwingine unaokubalika kisheria ambapo mtu au benki inatumia fedha zake katika kukodi vitu kama vile magari, majumba, ardhi, na kadhalika, ambavyo vikifanyiwa kazi huzalisha mali na kutoa faida. Benki za Kiislamu hujipatia faida kubwa kutokana na mtindo huu.(iv)Murabah
Huu ni utaratibu unaotumiwa katika kununua bidhaa kwa wingi kwa ajili ya kuwauzia wafanya biashara ambao waliofikiana kuwa bidhaa hizo zinunuliwe kwa ajili yao. Benki kutokana na uwezo wake inapanga na wafanya biashara kuwa inunue bidhaa nyingi kutoka ndani na nje ya nchi kwa jina lake kisha iwauzie wafanyabiashara hao kwa bei itakayoipatia benki faida. Pia benki kwa mtindo huu inaweza kununua mazao ya wakulima na kuyauza kwa walaji kwa faida.(v)Muqaradha
Mtindo huu wa Muqaradha humruhusu mtu au benki kununua “share” au “bonds” katika kampuni ya uzalishaji kwa mapatano ya kugawana faida au hasara kulingana na kiasi cha “share”.Kwa kufuata mitindo hii katika kuingiza fedha zake katika miradi ya uchumi, Benki za Kiislamu hupata faida kubwa hata zaidi ya kipato cha riba kinachopatikana katika benki za riba. Benki za Kiislamu nazo hugawa faida inayopatikana kwa wateja wake walioweka fedha zao kwenye benki.Uzuri wa benki za Kiislamu
Pamoja na benki za Kiislamu kutoa huduma zinazotolewa na kila benki kama tulivyoziorodhesha huko nyuma, kuna faida za ziada zinazopatikana kutokana na benki hizi kama ifuatavyo:Kwanza benki za Kiislamu huiokoa jamii na uchumi wake na madhara yote yanayosababishwa na riba.


Pili, Benki za Kiislamu huwaingiza katika uchumi na kuwainua hata wale ambao hawana hata rasilimali yoyote kwa mtindo wa Mudharabah. Hivyo ni kwamba, benki zinazoendeshwa kwa mikopo ya riba, haziwezi kukopesha fedha zake kwa mtu yeyote asiye na rasilimali yenye thamani sawa au zaidi ya mkopo ili atakaposhindwa kulipa ifilisiwe rasilimali hiyo. Kwa mtindo huu wa mikopo ya riba, ni matajiri tu wanaopata mikopo ya benki na masikini wasio na rasilimali yoyote huachwa hivyo hivyo na umasikini wao bila ya msaada kutoka benki wa kuwainua kiuchumi.Tatu, benki za Kiislamu huinua uchumi wa jamii, kutokana na umakini na tahadhari kubwa zinazochukua katika kuchagua na kuendesha miradi mbali mbali ya uchumi. Kwa kuwa benki zenyewe zinajiingiza katika uchumi, zinahakikisha kuwa miradi zitakazoichagua ni ile yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha faida kubwa na yenye uwezekano mdogo wa kusababisha hasara.