Maamrisho ya kushikamana nayo
Yale tunayoamrishwa kushikamana nayo ni haya yafuatayo: (i)Kumuabudu Allah (s.
(1) Maamrisho ya kushikamana nayo
Yale tunayoamrishwa kushikamana nayo ni haya yafuatayo:
(i)Kumuabudu Allah (s.w) Peke yake
Kumuabudu Allah (s.w) peke yake ndilo jukumu la kwanza kwa Muumini na hasa ndio lengo la kuumbwa binaadamu (rejea Qur-an 51:56). Kumuabudu Allah (s.w), ni kumtii kwa unyenyekevu katika kukiendea kila kipengele cha maisha ya binafsi na ya jamii.
(ii)Kuwafanyia wema na kuwahurumia wazazi Ni wajibu kwa Waumini kuwafanyia wema wazazi wao. Kuwafanyia wema wazazi ni pamoja na kuwafanyia yafuatayo:
(a) Kuwatii katika yale yote yanayowafikiana na sharia ya
Allah (s.w).Wazazi watakapowaamrisha watoto wao
wafanye mambo ambayo ni kinyume na amri za Allah (s.w) na Mtume wake, hawatapaswa kuwatii, bali watoto waumini wanapaswa kuwakatalia hao wazazi wao kwa adabu na heshima kubwa kwa kuwajibu kwa upole na kwa kauli nzuri.
(b)Kuwaheshimu wazazi kwa kuongea nao kwa upole na kwa huruma. Pia ni pamoja na kujiepusha na kujibizana nao, hata tu kuwagunia au hata kuwapuuza kwa ishara.
(c)Kuwahurumia wazazi kwa kuwapa msaada wowote wanaohitajia kwa kadiri ya uwezo wao, ila tu msaada huo uzingatie mipaka ya Allah (s.w) na Mtume wake.
(d)Kuwausia wazazi wao kumcha Allah (s.w) na kuwaombea dua na msamaha kwa Allah (s.w) kama tunavyoelekezwa na Allah (s.w) katika Qur-an:
"Mola wetu nighufirie mimi na wazazi wangu na wale wote wanaoamini siku ya Hisabu". (14:41)
Na tumemuusia mwanaadamu afanye wema kwa wazazi wake. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu. Na kubeba mimba yake hata kumwachisha ziwa; (uchache wake) ni miezi thalathini. Hata anapofikia baleghe yake na akawa mwenye umri wa miaka arubaini, (mtoto mwema) husema: - "Ee Mola wangu! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu na niwezeshe nifanye vitendo vizuri unavyovipenda, na unitengenezee watoto wangu; kwa yakini ninatubu kwako; na hakika mimi ni miongoni mwa waliosilimu (walionyenyekea)." (46:15)
(iii)Kutoa mali katika kuwasaidia wanaohitajia
Muumini anawajibika kutoa msaada wa mali na hali kuwapa wanaohitajia. Katika utaratibu wa kutoa msaada utaanza na jamaa zako wa karibu kisha ndio uwaangalie wahitaji wengine ikiwa ni pamoja na maskini, wasafiri walioharibikiwa na wengineo kama walivyoainishwa katika Qur-an (2:177), (4:36) na (51:19).Kama huna cha kutoa, angalau mliwaze huyo mwenye kuhitajia kwa kumpa maneno ya faraja na ya matumaini:
"Kauli njema na kusamehe ni bora kuliko sadaqa inayofuatishwa na udhia, na Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi na Mpole. (2:263)
(iv)Kutimiza vipimo
Waumini wanawajibika kuwa waadilifu wakati wa kuuziana kwa kukamilisha vipimo vya uzito, ujazo, urefu, n.k. Kufanya ujanja au ubabaishaji wowote katika vipimo ni katika makosa makubwa mbele ya Allah (s.w):
"Maangamizo yatawathubutikia wapunjao . Ambao wanapojipimia kwa watu hupokea (kipimo) kamili. Lakini wanapowapimia kwa (kipimo cha) vibaba au mizani (au vinginevyo) wao hupunguza. (83 1-3)
Je! Wao hawafikiri ya kwamba watafufuliwa; katika siku iliyo Kuu. (83:4-5)
Siku watakaposimama watu (wote) mbele ya Mola walimwengu wote?" (83:6)
(v) Kutimiza Ahadi
Ahadi ni deni ambalo linamlazimu Muumini kulilipa. Asiyetimiza ahadi kwa mujibu wa Qur-an (17:34) atakuwa ni mkosaji na siku ya Hukumu atasimamishwa kizimbani mbele ya Mahakama ya Allah (s.w) aulizwe juu ya ahadi aliyoivunja. Kuna aina mbili za ahadi; ahadi kuu na ahadi za kawaida.
Ahadi kuu ni ile iliyoichukua kila nafsi ya binaaadamu kuwa itamuabudu Allah (s.w) peke yake bila ya kumshirikisha na chochote. Rejea Qur-an (7:172-173). Waumini kila mara wanaikariri ahadi hii katika shahada na katika kila swala, hasa pale wanaposoma suratul-Faatiha na kuahidi "Wewe tu ndiye tunayekuabudu na Wewe tu ndiye tunayekuomba msaada". (1:5)
Ahadi za kawaida ni zile tunazoahidiana na binaadamu wenzetu katika kutekeleza mambo ya kheri. Ahadi za kufanya mambo maovu ni batili na hatuna budi kuzivunja pale tunapotanabahi.
Umeionaje Makala hii.. ?
Share On:
π1 Madrasa kiganjani π2 Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w) π3 web hosting π4 Tafasiri ya Riyadh Swalihina π5 Simulizi za Hadithi Audio π6 Kitau cha Fiqh
Post zinazofanana:
Muumini ni yule ambaye anazungumza ukweli
Ukweli ni katika sifa za waumini. Siku zote hakuna hasara katika kusema ukweli. Kinyume chake uongo ni katika madhambi makubwa sana.
Soma Zaidi...Dalili za kuwepo mwenyezi Mungu
Nguzo za Imani (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu)
Soma Zaidi...Mgawanyiko wa elimu usiokubalika katika uislamu
Ni mgawanyo upi wa elimu haukubaliki. Ni ipi elimul akhera na elimu dunia? (Edk form 1 Dhana ya elimu)
Soma Zaidi...Makemeo juu ya Zinaa na Hukumu kwa Wazinifu.
Tendo la zinaa ni tendo chafu kimaadili na Allah (s.
Soma Zaidi...