Vita vya Uhudi.
- Sababu ya kutokea vita vya Uhudi ni Maquraish kutaka kulipiza kisasi dhidi ya waislamu baada ya kushindwa katika vita vya Badri.
- Maquraish waliandaa msafara wa biashara wenye thamani ya Dirham 300,000 kuelekea Iraq kama maandalizi ya kulipiza kisasi vita vya Badri.
- Kikosi cha waislamu kikiongozwa na Zaid bin Harith (r.a) kiliteka msafara huo na kuchukua mali yenye thamani ya Dirham 100,000 na mateka 2.
- Vita vilipiganwa siku ya Jumamosi, mwezi 15 Shawwal, mwaka wa 3 A.H (625 A.D) katika milima ya Uhudi nje ya mji wa Madinah.
- Waislamu walikuwa 700 (baada ya wanafiki 300 kurudi nyuma wakiongozwa na Abdullah bin Ubayyi) na Maquraish wakiwa askari 3,000 waliojizatiti kivita, (700 wamevaa mavazi ya chuma), farasi 200 na ngamia 3,000.
- Kwa waislamu kiongozi alikuwa Mtume (s.a.w) na kwa Maquraish viliongozwa na Hindu bint Utbah mkewe Abu Sufyan.
- Mtume (s.a.w) aliteuwa kikosi cha watu 50 wakiongozwa na Abdullah bin Jubeir kukaa juu ya mlima ili kulinda kikosi cha maadui kikiongozwa na Khalid bin Walid.
- Vita vilipoanza waislam walipata ushindi lakini baadae kugeuka kipigo baada ya waislamu 43 kuondoka mlimani na kupelekea Mtume kuvunjwa meno 2.
- Waislamu 70 waliuuawa akiwemo shujaa Hamza bin Abdi Muttalib (r.a) aliyeuliwa na mtumwa Wahshi bin Harbi aliyeandaliwa na Hindu bint Utbah.
Mafunzo yatokanayo na Vita vya Uhudi.
1.Lengo la maadui wa Uislamu na waislamu kupigana ni kuwaangamiza wao, kuharibu miji yao na mali zao pia. Hivyo ni wajibu waislamu kuwa na tahadhari muda wote kupambana na maadui wao.
2.Kushauriana katika kupanga mambo ni jambo la busara sana, kama alivyoshauriana Mtume (s.a.w) juu ya sehemu ya kupiganwa vita vya Uhudi.
Rejea Qur’an (3:159) na (3:166-167).
3.Tunajifunza pia ni wajibu waislamu kutumia mbinu, ujuzi, uzoefu, na jitihada za kivita pamoja na kuwa wanapata msaada wa Mwenyezi Mungu (s.w).
Rejea Qur’an (8:60).
4.Msaada wa Mwenyezi Mungu (s.w) kwa waislamu unapatikana pale tu waislamu watakapotii amri zake na wakapigania dini vilivyo.
Rejea Qur’an (3:151-152).
5.Kuvunja na kutotii amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake hupelekea kutofikia mafanikio hata kama watajizatiti na kufanya jitihada ipasavyo.
Rejea Qur’an (3:152), (3:165) na (33:36).
6.Tunajifunza pia, makosa ya watu wachache yasipuuzwe na kufumbiwa macho bali yarekebishwe kwani athari yake itasibu jamii nzima.
Rejea Qur’an (8:25).
7.Mwenyezi Mungu (s.w) anatukumbusha kuwa pepo haipatikani kwa kutamani, lele mama na ushabiki bali, kufanya jitihada ya kweli.
Rejea Qur’an (3:142-150), (3:156-160) na (3:169-171).
8.Msamaha na nusura ya Mwenyezi Mungu (s.w) upo karibu kwa waislamu pindi watakapotubia na kurejea kwake na kupambana na maadui ipasavyo.
Rejea Qur’an (3:152-154), (3:166-167) na (3:139-141).
9.Ushindi wa waislamu katika vita unatoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w) na sio kutokana na ubora wa silaha na wingi wa askari.
Rejea Qur’an (3:123-124), (8:42-45).
10.Choko choko na mbinu za maadui dhidi ya Uislamu na waislamu ni zenye kuendelea na hazitaisha kamwe hadi siku ya Qiyama.