Mafunzo ya sura zilizochaguliwa
Quran (EDK form 2: dhana ya elimu ya uislamu)
Mafunzo ya sura zilizochaguliwa.
- Suratul-Lahab (111): Imeteremshwa Makka; Ina Aya Tano.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
- Imeangamia mikono ya Abulahab naye amekwisha angamia.
- Haitamfaa mali yake wala alivyovichuma (watoto).
- (Atakapokufa) Ataingia moto wenye muwako (mkubwa kabisa).
- Na mkewe (ni) mchukuzi wa kuni (za fitina).
- (Kana kwamba) Shingoni mwake iko kamba iliyosokotwa (anayechukulia kuni za fitina).
Mafunzo ya sura kwa ufupi.
- Binaadamu siku zote huamua kumkanusha Mwenyezi Mungu (s.w) kwa kibri na jeuri.
- Mali na watoto havina msaada wowote pindi inapokuja adhabu ya Mwenyezi Mungu (s.w).
- Watu waovu na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu (s.w) wana mwisho mbaya wa kuishia motoni.
- Maadui wa Uislamu na waislamu siku zote hawakati tamaa katika kuzuilia watu kuingia na kuufuata Uislamu.
- Uchochezi, fitina na uasi ni miongoni mwa makosa makubwa yenye kuangamiza.
- Suratul-Nnasr (110): Imeteremshwa Madinah Ina Aya Tatu.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
- Itakapofika Nusura ya Mwenyezi Mungu na Kushinda.
- Na ukawaona watu wanaingia katika Dini ya Mwenyezi Mungu makundi makundi.
- Basi (hapo) mtakase Mola wako pamoja na kumsifu na umuombe magh’fira (msamaha) hakika Yeye ndiye apokeaye toba.
Mafunzo ya Sura kwa Ufupi.
- Nusura na mafanikio hutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w) pekee.
- Baada ya nusura na ushindi hatuna budi kumshukuru, kumtukuza na kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu (s.w) bila ya kujivuna.
- Katika kufanya juhudi, hatuna budi kuchunga na kutii ipasavyo maarisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
- Nusura na mafanikio ya kweli huja baada ya juhudi za dhati za kibinaadamu kufanyika na kumtegemea Mwenyezi Mungu (s.w) vilivyo.
- Mafanikio ya kweli sio kujilimbikizia mali na anasa za dunia tu, bali ni kuipigania Dini ya Mwenyezi Mungu (s.w) ipasavyo.
- Suratul-Kaafiruun (109): Imeteremshwa Makkah, Ina Aya Sita.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
- Sema: Enyi Makafiri.
- Siabudu mnachoabudu.
- Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu.
- Wala sitaabudu mnachoabudu.
- Wala nyinyi hamtaabudu ninayemuabudu (mimi).
- Nyinyi mna dini yenu na mimi nina dini yangu.
Mafunzo ya Sura kwa Ufupi.
- Dini ni utaratibu wowote ule wa maisha anaoufuata mtu.
- Kuna dini nyingi hapa Ulimwenguni, Ukafiri nao ni dini.
- Hakuna uwezekano wa mwanaadamu kufuata dini (utaratibu wa maisha) za ya moja kwa wakati moja, Uislamu na mifumo mingine.
- Waislamu wa kweli ni wale wasiochanganya haki na batili kwa kuwahofia makafiri.
- Ni wajibu kuitangaza haki kwa wengine bila kuhofia chuki na uadui wao dhidi ujumbe uliowapa.
- Suraul-Kawthar (108): Imeteremshwa Makka, Ina Aya Tatu.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
- Hakika tumekupa kheri nyingi.
- Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje (kwa ajili yake pia).
- Hakika adui yako ndiye atakayekuwa mkiwa (atakatikiwa na kila kheri).
Mafunzo ya Sura kwa Ufupi.
- Mafanikio hayapimwi kwa wingi wa mali na watoto, bali ni kuridhiwa na Mwenyezi Mungu (s.w).
- Hakuna neema kubwa kama kujaaliwa kuupokea Uislamu, kuuelewa, kuufuata vilivyo na kuufikisha kwa wengine.
- Hatuna budi kumuabudu Mwenyezi Mungu (s.w) peke yake ipasavyo na kufanya kila jambo kwa ajili yake tu.
- Maadui na Wapinzani wa Uislamu ndiyo wenye kupata khasara na kufedheheka duniani na Akhera pia.
- Ushindi na mafanikio hupatikana kwa waislamu baada ya kutii na kufuata maamrisho ya Uislamu vilivyo.
- Suratul-Maaun (107): Imeteremshwa Makka, Ina Aya Saba.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
- Je, Unajua yule anayekadhibisha dini (asiyeamini malipo ya Akhera)?
- Huyu ni yule anayemnyanyasa yatima.
- Wala hajihimizi (yeye wala wengine katika) kuwalisha maskini.
- Basi adhabu kali itawathubutikia wanaoswali.
- Ambao wanapuuza (maamrisho ya) swala zao.
- Ambao hufanya riyaa (ya kujionyesha kwa watu).
- Nao hunyima misaada (midogomidogo kwa wanaohitajia).
Mafunzo ya Sura kwa Ufupi.
- Imani katika Uislamu hudhihirishwa katika matendo ya mtu na sio kauli au maneno tu.
- Kuwadhulumu, kuwasimanga au kuwatendea uovu wowote mayatima na wenye shida ni katika makosa makubwa.
- Swala ni lazima itekelezwe kwa kuzingatia ipasavyo nguzo, sharti zake pamoja na khushui (unyenyekevu).
- Kutenda jambo lolote kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu (s.w) ndio uhai wa ibada ya muumini.
- Maisha ni jambo la kijamii ambalo linahitajia watu kuishi pamoja kwa kusaidiana inapobidi.
- Muumini wa kweli ni yule aliyemwepesi kutoa misaada kwa wanaadamu wenzie na mwenye kujali matatizo ya wengine yanapowapata.
- Suratul - Qureish (106): Imeteremshwa Makkah, Ina Aya Nne.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
- Ili kuwafanya Maqureish waendelee.
- Waendelee na safari zao za wakati wa kusi (kwenda Yemen) na wakati wa kaskazi (kwenda Sham ndiyo maana tukajaalia jeshi la ndovu kushindwa).
- Basi na wa muabudu Bwana wa Nyumba hii (Al-Kaaba).
- Ambaye amewalisha (wakati wa) katika njaa na anawapa amani (wakati wa) katika khofu.
Mafunzo kwa Ufupi.
- Kwa hakika anayelisha na kulinda ni Mwenyezi Mungu (s.w) peke yake.
- Amani, Usalama na Ustawi wa kweli wa jamii hutokana na kushikamana na amri za Mwenyezi Mungu (s.w).
- Shukrani za kweli kwa Mwenyezi Mungu (s.w) ni kumuabudu ipasavyo.
- Maingiliano ya Mataifa kibiashara ni katika neema za Mwenyezi Mungu (s.w).