Hii ndio namna ya kuswali kama alivyoswali Mtume s.a.w

Mtume (s.

Hii ndio namna ya kuswali kama alivyoswali Mtume s.a.w

Mtume (s.a.w) ametuagiza katika Hadith maarufu kuwa tuswali kama alivyokuwa akiswali. Hivyo katika sehemu hii tutajitahidi kuonesha utekelezaji wa swala hatua kwa hatua kwa kurejea Hadith Sahihi za Mtume (s.a.w):


1. Nia na Takbira ya kuhirimia



Nia ni kudhamiria moyoni kuwa unaswali, swala unayoikusudia kisha unaanza swala kwa kusema: 'Allaahu Akbar' Allah ni Mkubwa kwa kila hali'. Wakati wa kuhirimia swala ni sunnah kuinua viganja vya mikono,mkabala na mabega. Kuhusu unyanyuaji wa mikono mkabala na mabega imeripotiwa kuwa Mtume (s.a.w) alikuwa akifanya hivyo katika sehemu nne tofauti:
1. Wakati wa kuhirimia swala (kuanza swala).
2. Wakati anaposema Allaahu Akbar kwa ajili ya rukui.
3. Wakati anaposimama kutoka kwenye rukuu.
4. Wakati anaposimama kutoka kwenye tahiyyatu ya kwanza ili kuendelea na rakaa ya tatu.


Hii tunaipata katika Hadith aliyosimulia Abdullah bin 'Umar kuwa: 'Mtume (s.a.w) aliposimama kwa ajili ya swala alinyanyua mikono yake mkabala na mabega yake na kisha kuhirimia (kusema Allahu Akbar). Alipotaka kurukuu alinyanyua mikono kama alivyofanya kwanza na aliposimama kwa ajili ya itidali alifanya hivyo hivyo na alisema Allah anamsikia yule anayemsifu. (Bukhari, Muslim na Bayhaqi). Nafa'a(r.a) ameeleza kwamba Ibn 'Umar (Abdullah)(r.a) aliposimama kwa ajili ya rakaa ya tatu alikuwa akinyanyua mikono; jambo ambalo alilihusisha na Mtume (s.a.w). (Bukhari, Abu Dawud, Nasai).


Baada ya kuhirimia swala mwenye kuswali hushusha mikono yake na kuiweka kifuani, mkono wa kulia ukiwa juu ya mkono wa kushoto kwa mujibu wa Hadith zifuatazo: Hulab At-Tai(r.a) amesimulia: 'Nilimuona Mtume (s.a.w) akiswali hali ameweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua chake.' (Ahmad na At-Tirmidh)


Naye Wail bin Hijr (r.a) ameripoti: 'Niliswali pamoja na Mtume (s.a.w) na aliweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua chake'. (Ahmad na At-Tirmidh).


Imamu Abu Dawud na Nasai wamepokea kutoka kwa Ibn Khuzaimah kuwa Mtume (s.a.w) alipokuwa akiswali alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya kiwiko (wrist) cha mkono wa kushoto na sehemu ya mkono inayofuatia kiganja


2.Kusoma Dua ya Kufungulia Swala
Kusoma dua ya kufungulia swala ni sunnah. Katika Hadithi ya Bukhari na Muslim iliyosimuliwa na Abu Hurairah (r.a), baada ya kuhirimia swala Mtume (s.a.w) alikuwa akileta dua ifuatayo: 'wajahtu wajhi lilladhi fatwaras-samaawat wal-ardha hanifam-muslima wamaa ana minal-mushrikina. Inna swalatiy wanusukii, wamah-haya, wamaamatiy, lillahi rabil-alamiina laa sharikalahu wabidhalika umirtu wa-ana minal-muslimiina.'Nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi. Nimeacha dini za upotovu. Mimi si miongoni mwa washirikina. Hakika swala yangu (na ibada zangu zote) na uzima wangu na kufa kwangu (yote) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, bwana (Rabbi) wa walimwengu wote. Hana mshirika wake. Na haya ndio niliyoamrishwa na mimi ni wa kwanza walio jisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu. (6:79, 162-163)


3. Kupiga Audhu Billah Kabla ya kuanza kusoma Qur-an ni amri ya Allah (s.w) kujikinga na sheitwani kama inavyodhihirika katika aya ifuatayo: 109 'Na ukitaka kusoma Qur-an piga Audhu billah (jikinge) kwa Allah (akulinde) na Sheitwani aliyefukuzwa (kwenye Rehema). (16:98) Hivyo tuanze kusoma Qur-an kwa kusema 'A'udhu-billahi minash-shaytwanir- Rajiim' Najikinga kwa Allah na sheitwan aliyefukuzwa-kwenye Rehma yako


4. Kusoma Suratul-Fatiha Kusoma Suratul-Fatihah ni nguzo ya tatu ya swala na ndio nguzo kubwa ya swala. Tunasoma suratul-Fatiha kama ifuatavyo:- Bismillahir Rahmaanir Rahiim (1) Alhamdu liLLahi rabbil-'Aalamiin (2). Rrahmaanir Rahiim (3) Maaliki yaumiddiin (4) Iyyaakana 'abudu waiyyaaka nasta'iin (5) Ih dinasw-swiraatwal mustaqiim (6) Swiraatwa lladhiina an 'amta 'alaihim; ghairil maghdhuubi 'alaihim wala dhw-dhwaaliin (7)


Tafsri:
(1) Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu: (2) Shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola wa Walimwengu wote: (3) Mwingi wa Rehema mwenye kurehemu (4) Mwenye kumiliki siku ya malipo: (5) Wewe tu ndiye tunayekuabudu, na wewe tu ndiye tunaye kuomba msaada: (6) Tuongoze njia iliyonyooka: (7) Njia ya wale uliowaneemesha; siyo (ya wale ) waliokasirikiwa, wala ya wale waliopotea
5. Kusoma Qur-an baada ya Suratul-Fatiha Katika rakaa ya kwanza na ya pili ni Sunnah baada ya kusoma Suratul-Fatiha kuleta Surah au aya nyingine za Qur-an


6.Kurukuu
Baada ya kusoma Suratul-Fatiha na Surah nyingine, au baadhi ya aya katika sura nyingine unasema Allahu-akbar kisha unarukuu (kuinama). Rukuu ni nguzo ya swala pamoja na kujituliza humo. Katika rukuu ni sunnah kumsabihi Allah (s.w) kwa kusema kimya kimya mara tatu au zaidi 'Subhana Rabbiyal'Adhiim' 'Utukufu ni wako Ee Bwana (Mlezi) wangu Uliye mkuu'


7.Kuitidal
Kuitidali ni kusimama wima kutoka kwenye rukuu, ni sunnah kusema wakati wa kunyanyuka maneno haya:'sami'a llahu liman hamidahu' Mwenyezi Mungu anamsikia kila mwenye kumhimidi. Na baada ya kusimama sawa ni sunnah kusema 'rabbanaa walakal-hamdu'ewe mola wetu sifa zote za ukamilifu ni zako. Pia ni sunnah kusema maneno haya 'rabbanaa walakal-hamdu mil-as-samaawati wamil-al-ardhi wamil-amashi-ita minshai-in ba'adah' Ewe Mola wetu sifa zote za ukamilifu ni za kwako, kutoka mbinguni, kutoka ardhini na katika vitu vyote vilivyo baina yao (mbingu na ardhi) na kutoka katika vinginevyo unavyo viridhia


8.Kusujudi
Ni nguzo pamoja na kujituliza katika sujudi. Mkusujudi ni kuvituliza chini viungo saba kwa utaratibu wa swala. Vingo hivyo ni , paji a uso, viganya viwili vya mikono, magoti mawili na matumbo ya nyayo za vidole vya miguuni.viungo vyote hivi vinatakiwa vielekee kibla. Paji la uso ni pamoja na pua iguse chini.utasema kwenye sijda 'subhaana rabbiyal-a'alaa' utukufu ni wa kwako Mola uliye tukuka.


9.kukaa baina ya sijda mbili
Hiki ni kitako kinachopatikana baada ya kutoka kusujudi. Sifa ya kikao hiki ni kukalia unyayo wa mguu wa kushoto na kuweka mikono miwili juu ya mapaja. Ni sunnah kusema maneno haya: 'rabbigh-firliy warhamnii wa'afinii warzuqniy'Ewe Mola wangu nisamehe, na unirehemu, na unipe afya na uniruzuku


10.kikaa tahiyyatu
Katika kukaa Thiyyatu mtume alikuwa akikalia futi la mguu wa kushoto na kusimamisha futi la mguu wa kulia na katika tahiyyatu ya mwisho alikaa chini na kuulaza mguu wa kushoto katika uvungu wa mguu wa kulia na alisimamisha futi la mguu wa kulia, katika vikao vyote hivyo viwili,


Mtume (s.a.w) alivilaza viganja vyake juu ya mapaja karibu na magoti kama tunavyoelezwa katika hadith ifuatayo: Abdullah bin Jubair(r.a) ameeleza kuwa wakati Mtume (s.a.w) alipokaa tahiyyatu, alikuwa akiweka kiganja chake cha mkono wa kulia juu ya paja lake la kulia na kiganja cha mkono wa kushoto juu ya paja la mguu wa kushoto na alikuwa akinyoosha kidole chake cha shahada (wakati wa k u s e m a , ' A s h - h a d u anllaaillaha illallah) na kukiegemeza juu ya kidole gumba na alikuwa akiweka kiganja chake cha mkono wa kushoto juu ya goti lake (la mguu wa kushoto). (Muslim).


11.Kusoma Tahiyyatu
Kusoma tahiyyatu ni nguzo ya swala. 'Tahiyyatu' ina maana ya 'Maamkizi', ukiwa umekaa kikao cha tahiyyatu unaleta maamkizi kama ifuatavyo: 'Attahiyyaatu lillaah, wasw-swalawaatu, watwa-yyibaatu, assalaamu 'alaika ayyuhannabiyyu, warahmatullaahi wabarakaatuhu, assalaamu 'alay-naa wa-'alaa 'ibaadillaahi swswaalihiina. Ash-hadu an-llaailaaha illallaahu wa-ash-hadu anna Muhammadan 'abduhuu warasuuluhu'. 'Maamkizi yote ni ya Allah, na swala zote na yote mazuri, Amani iwe juu yako, ewe Mtume na Rehma na Baraka za Allah. Na amani iwe juu yetu na juu ya waja wema wa Allah. Ninashuhudia kuwa hapana Mola ila Allah. Na ninashuhudia kuwa Muhammad ni Mja na, ni Mtume wake'. (Muslim).


12. Kumswalia Mtume (s.a.w).
Kumswalia Mtume (s.a.w) ni nguzo ya swala inayofuatia baada ya kusoma Tahiyyatu. Kumswalia Mtume si faradhi katika swala tu bali pia ni faradhi kumswalia kila anapotajwa kwa jina lake. Msisitizo wa amri ya kumswalia Mtume unaonekana katika aya ifuatayo:


'Hakika Mwenyezi Mungu anamteremshia Rehema Mtume; na Malaika wake (wanamuombea dua). Basi; enyi Mlioamini msalieni (Mtume, muombeeni Rehema) na amani'. (33:56)


Pia hadithi zifuatazo zinasisitiza umuhimu wa kumswalia Mtume (s.a.w) kila atajwapo na kila mtu apatapo wasaa. Ali (r.a) amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Bakhili ni yule anayesikia nikitajwa, lakini haniswalii. (hanitakii rehma). (Tirmidh).


Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: 'Anayenitakia Rehma (anayeniswalia) mara moja, Allah humrehemu mara kumi'. (Muslim).


'Ibn Mas'ud amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Atakayekuwa kipenzi changu katika watu, katika siku ya Kiama atakuwa ni yule aliye mbele kuliko wote katika kunitakia Rehma (kuniswalia). (Tirmidh).


Namna ya kumswalia Mtume (s.a.w) imeelezwa katika Hadithi nyingi lakini iliyomashuhuri katika hizo ni ile iliyosimuliwa na Abdur- Rahman bin Ubaidillah(r.a) na kupokelewa na Maimamu wote wa Hadithi kuwa Mtume (s,.a.w) ametufundisha tumswalie (tumtakie Rehma) kama ifuatavyo;


'Allahumma swalli 'alaa muhammad wa'alaa aliy Muhammad kamaa swallaita 'alaa ibraahima wa'alaa ali ibraahim innaka hamiidum-majid. Wabaaik 'alaa muhammad wa'alaa ali muhammad kamaa barakta 'alaa ibraahima wa'alaa ali ibraahima innaka hamiidum-majid'


Ewe Mola mrehemu Muhammad na wafuasi wake kama ulivyomrehemu Ibrahim na wafuasi wake hakika wewe ni mtukufu na msifiwa wa haki. Ewe Mola mbariki Muhammad na wafuasi wake kama ulivyombariki Ibraahim na wafuasi wake hakika wewe ni wewe ni mtukufu na msifiwa wa haki.


12.Dua kabla ya salamu
Ni sunnah kuleta dua kabla ya salamu. Dua hizi ni nyingi ila miongoni mwanzo ni
Dua aliyotufundisha Mtume (s.a.w) kwa msisitizo mkubwa kama tunavyofahamishwa katika Hadithi ya Muslim, iliyosimuliwa na Ibn Abbas, ni hii ifuatayo: Allahumma Inni-audhubika min-'adhaabi-lqabri,Wa-auudhubika min fitnatil masiihi-ddajjaal, Wa-auudhubika min fitnatil-mahyaa wal-mamaati, 'Ee Allah najikinga kwako kutokana na adhabu ya kabr, na najikinga kwako kutokana na fitina za masiihi Ddajjaal na najikinga kwako kutokana na matatizo ya maisha na mauti.


Sijidat-Sah-wi (Sijda ya kusahau)
Sijdat Sah-wi ni sijidah anayoileta mtu kabla ya kutoa salaam ili kufidia kitendo cha sunnah alicho kisahau kwa mfano kusahau kukaa tahiyaatu ya kwanza.Vile vile mtu akisahau au akikosea jambo lolote ambalo halibatilishi swala kwa mfano akaswali rakaa tano badala ya rakaa nne kwa swala ya Adhuhuri. Kabla hajamaliza swala alete sijidat Sahau. Hivi ndivyo tunavyojifunza kutokana na Hadithi zifuatazo: Abdullah bin Mas'ud (r.a) amesimulia: Mtume wa Allah alituswalisha Adhuhuri rakaa tano.Tukamuuliza kama pameamrishwa na Mwenyezi Mungu kurefushwa swala akajibu, La! Tukamuambia: 'Umetuswalisha rakaa tano. Akasema (Mtume): Mimi ni binaadamu kama nyinyi, nakumbuka kama mnavyokumbuka na nasahau kama mnavyosahau. Kisha akasujudu sijdah mbili zikawa ni fidia kwa kusahau. (Bukhari na Muslim).


Muhimu:
Kumbuka kuwa sijda hii Mtume (s.a.w) aliileta baada ya kutoa salaamu na baada ya kukumbushwa. Abdullah bin Buhaymah (r.a) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) aliswalisha swala ya adhuhuri, akasimama baada ya rakaa mbili, alipomaliza swala akasujudu mara mbili huku akisema: 'Allah Akbar' katika kusujudu na katika kuinuka, wakati amekaa kabla ya kutoa salaam, na watu wakasujudu pamoja naye. Hii ilikuwa ni kufidia ile tahiyyatu ya mwanzo aliyoisahau'. (Muslim)


14. kutoa salamu.
Kutoa salamu ni nguzo katika nguzo za swala. Ukamilifu wa kutoa salamu ni kusema 'as-salaamu alykum warahmatullahi wabarakaatuh' salamu zipo mbili yakwanza utatoa upande wa kulia na ya pili utatoa upande wakushoto. Sifa ya kugeuka kwa kutoa salamu ni kuwa utageuka mpaka mashavu yawze kuonekana kwa mtu aliye nyuma.


Lugha ya Swala Lugha ya swala,
kuanzia kwenye Takbira ya kuhirimia Swala mpaka kumalizia swala kwa Salaam, ni Kiarabu. Hekima yake iko wazi. Kiarabu ndio lugha ya Qur-an tukufu na kwa hiyo ndio lugha rasmi ya Kiislamu inayowaunganisha Waislamu wote ulimwenguni. Waislamu ni umma mmoja tu na Waislamu wote ni ndugu moja wasio baguana kwa lugha, rangi, taifa wala ubaguzi mwingine wa aina yoyote ile.Muislamu yeyote anaweza kuwa Imamu mahali popote ilimradi tu awe anatekeleza masharti ya Uimamu. Muislamu hana msikiti maalum. Misikiti yote ni yake na anaweza kuswali kwenye msikiti wowote ulimwenguni bila ya kupata tatizo lolote la lugha. Kwa sababu hii kila Muislamu inabidi ajifunze kiasi cha uwezo wake kutamka, kwa Kiarabu yale yote tuyasemayo katika swala..


Dua na Dhikri Baada ya Swala
Ni vizuri mara Muislamu anapomaliza kuswali kama hana dharura yoyote asiondoke bila ya kuleta Dhikri na dua kama alivyofundisha Mtume (s.a.w), kwani zina umuhimu mno katika kumsaidia mja kufikia lengo la swala na lengo la kuumbwa kwake kwa ujumla iwapo atayafahamu na kuyazingatia yale anayoyatamka. Kutokana na Hadithi iliyosimuliwa na Samura bin Jandab(r.a) na kupokelewa na Bukhari(r.a), baada ya swala Mtume (s.a.w) aliwageukia Waislamu aliokuwa akiwaswalisha. Kisha aliomba maghfira (msamaha) mara tatu na kuongezea maneno yaliyoelezwa katika Hadithi zifuatazo: Thawban (r.a) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) alipomaliza swala aliomba maghfira (msamaha) mara tatu kwa kusema: Astagh-firullah (Mara tatu) Ninaomba msamaha kwa Allahh na kusema 'Allahumma Antassalam waminkas-salaam Tabaarakta YaaDhal jallaali Wal-ikraam.' Ewe Allah, wewe ni Amani, na kwako ndiko iliko Amani. Wewe ndiye Mbariki Ewe Mwenye Utukufu na Heshima (Muslim)


Baada ya nyiradi hizi, ni vizuri pia kuomba dua yoyote kulingana na haja zako kwa lugha yoyote. Jambo hili la kuomba dua baada ya swala, umuhimu wake unadhihirika katika hadithi ifuatayo: Abu Umamah amesimulia kuwa: Iliulizwa: Ee Mtume wa Allah. ni dua gani ambayo hukubaliwa zaidi?h (Mtume) alijibu: (moja) ni ile ya katikati ya nusu ya pili ya usiku na (pili) kila baada ya swala ya faradhi. (Tirmidh)


Hivyo ni jambo la msingi mno kuomba dua yoyote kila baada ya swala na dua zilizo nzito zaidi ni zile zilizomo kwenye Qur-an na hadithi za Mtume (s.a.w). Kwa mfano ni vizuri kila baada ya swala, au baada ya dhikri zilizotajwa tuombe dua ifuatayo: Rabii ij'alnii muqiimas-swalaati wamindhurriyyatii Rabbana Wataqabbal du'aaai. Mola wangu! Nijaalie niwe msimamishaji swala, na kizazi changu! (Pia kiwe hivi). Mola wetu! Na upokee maombi yangu mengine... (14:40-41).





                   




Je! umeipenda hii post?
Ndio            Hapana            Save post

Kama unahitaji kuuliza maswali Bofya hapa

Mwandhishi Tarehe 2018-08-01     Share On Facebook or Whatsapp Imesomwa mara 422


Download our Apps
👉1 Kitau cha Fiqh     👉2 Kitabu cha Afya     👉3 Madrasa kiganjani     👉4 kitabu cha Simulizi    

Post zifazofanana:-

Hadithi Ya 22: Je, Nikiswali Swalah Za Fardhi, Nikafunga Ramadhaan
Soma Zaidi...

SIRI YA KIFO INAFICHUKA
Soma Zaidi...

Sharti za kusihi kwa funga
Soma Zaidi...

vita vya ahzab, sababu ya kutokea vita hivi na mafunzo tunayoyapata
Vita vya Ahzab- Maquraish waliungana na mayahudi, wanafiki na makabila mengine ya waarabu baada ya kuona kuwa wao peke yao hawawezi kuufuta Uislamu. Soma Zaidi...

NAMNA AMBAZO DUA HUJIBIWA
NAMNA AMBAYO ALLAH HUJIBU DUA. Soma Zaidi...

Historia ya Luqman mtu aliyesifika kuwa na Hikma
Luqman ni katika watu wema kabisa waliopita zama za nyuma. Soma Zaidi...

Mtazamo wa Uislamu juu ya usawa kati ya mwanaume na mwanamke
Soma Zaidi...

Hifadhi ya Mwanamke na Maadili ya Jamii
(c) Hifadhi ya Mwanamke na Maadili ya JamiiKimaumbile wanaadam kama walivyo wanyama, wamejaaliwa kuwa na mvuto wa kimapenzi kati ya mume na mke ili kuwawezesha kutekeleza wajibu mkubwa wa kuzaana na kuendeleza kizazi. Soma Zaidi...

Historia ya Watoto Wawili wa Nabii Adam
'Na wasomee khabari za watoto wawili wa Adam kwa kweli, walipotoa sadaka, ikakubaliwa ya mmoja wao na ya mwingine haikukubaliwa Akasema (yule asiyekubaliwa sadaka yake): 'Nitakuua'. Soma Zaidi...

Kumuandaa Maiti kabla ya kufa ama kukata roho
Soma Zaidi...

Nini maana ya Uchoyo, na madhara yake kwenye jamii
31. Soma Zaidi...

Nini maana ya Kushahadia nguzo ya kwanza ya uislamu
Soma Zaidi...